Chenene
Chenene | ||||||||||||||||||
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
Chenene wa Kawaida (Gryllotalpa africana)
| ||||||||||||||||||
Uainishaji wa kisayansi | ||||||||||||||||||
| ||||||||||||||||||
Ngazi za chini | ||||||||||||||||||
Nusufamilia 2, jenasi 8; jenasi 1 na spishi 17 katika Afrika:
|
Chenene ni wadudu wa jamii ya nyenje-ardhi katika familia Gryllotalpidae wa oda Orthoptera. Miguu ya mbele imetoholewa kwa kuchimba na ina umbo la beleshi lenye meno.
Maelezo
haririChenene hutofautiana kwa ukubwa na mwonekano, lakini wengi wana ukubwa wa wastani baini ya wadudu. Kwa kawaida urefu wao ni kati ya sm 3.2 na 3.5 katika wapevu. Wametoholewa kwa maisha ya chini ya ardhi. Wana umbo la mcheduara na wamefunikwa kwa nywele nyingi laini. Kichwa, miguu ya mbele na protoraksi zina deraya zito ya khitini, lakini fumbatio ni nyororo kiasi. Kichwa hubeba vipapasio viwili kama nyuzi na macho kama shanga ndogo. Jozi mbili za mabawa hufungika bapa juu ya fumbatio. Katika takriban spishi zote mabawa ya mbele ni mafupi na yameviringa, na mabawa ya nyuma ni kama viwambo na hufikia au kuzidi ncha ya fumbatio. Walakini, katika spishi nyingine mabawa ya nyuma yamepunguka kwa urefu na mdudu hawezi kuruka angani. Miguu ya mbele imekuwa bapa ili kuchimba, lakini miguu ya nyuma imeumbwa kama miguu ya nyenje-ardhi. Walakini, miguu hii imetoholewa zaidi kwa kusukuma mchanga badala ya kuruka, ambayo wanafanya mara chache na vibaya.
Mzunguko wa maisha
haririChenene hupitia metamofosisi isiyo kamili. Mayai hutoa tunutu wanaofanana na wapevu isipokuwa kukosa kwa mabawa na viungo vya uzazi. Hupitia mfululizo wa hatua na maambuaji ambazo idadi yao inaweza kufika 10. Pedi za mabawa zinakuza kubwa zaidi baada ya kila ambuaji.
Baada ya kupandana jike anaweza kupitia kipindi cha wiki 1-2 kabla ya kutaga mayai. Anachimba ndani ya ardhi kwa kina cha sm 30 (kwenye maabara sm 72 imeonwa) na kutaga kishada cha mayai 25 hadi 60. Kisha jike wa Neoscapteriscus hujitoa akiziba kifungu cha kuingilia, lakini katika spishi za Gryllotalpa na Neocurtilla jike ameonekana kubaki katika chumba kinachoungana ili kuchunga kishada. Vishada vingine vinaweza kufuata ndani ya miezi kadhaa kulingana na spishi. Lazima mayai yatagwe kwenye mchanga wenye unyevu ili kukomaa. Mayai hutoa tunutu katika wiki chache na wakikua hao hula maada ya mimea ama chini ya ardhi au juu ya uso wake.
Wapevu wa spishi kadhaa za chenene wanaweza kuhama umbali wa hadi km 8 wakati wa msimu wa uzalishaji. Chenene hukiakia takriban mwaka mzima, lakini katika tabianchi baridi hupitia majira ya baridi kama tunutu au wapevu wakitulia chini ya ardhi na kuwa wamilifu tena wakati wa majira ya kuchipua.
Mwenendo
haririWapevu wa spishi nyingi za chenene wanaweza kuruka angani kwa nguvu, ikiwa sio kwa wepesi, lakini madume hufanya hiyo mara chache tu. Kwa kawaida majike huruka juu muda mfupi baada ya machweo na huvutiwa na maeneo ambapo madume hupiga sauti, ambayo hufanya kwa karibu saa moja baada ya machweo. Hii inaweza kuwa ili kupandana au majike wanaweza kuvutiwa na uwepo wa makazi wa kutaga mayai, kama inavyoonyeshwa na idadi ya madume waliopo na kupiga sauti karibu.
Uchimbaji
haririChenene huishi chini ya ardhi takriban saa zote, ambapo huchimba penyo za aina mbalimbalii kwa shughuli kuu za maisha, pamoja na kujilisha, kuwakimbia mbuai, kuvutia wenzi (kwa njia ya kupiga sauti), kupandana na kutaga mayai.
Penyo zao kuu hutumiwa kwa kujilisha na kutoroka. Wanaweza kujichimba chini ya ardhi kwa haraka sana na wanaweza kusonga mbele na nyuma katika penyo zilizopo kwa kasi kubwa. Mbinu yao ya kuchimba ni kunanua ardhi pande mbili kwa miguu yao ya mbele yenye nguvu inayofanana na mabeleshi. Miguu hiyo ni mipana na bapa na ina meno na deraya nzito (kutikula ni ngumu na nyeusi).
Madume huvutia wenzi kwa kujenga penyo kwa umbo maalum ambamo hupiga sauti. Upenyo wa spishi za Gryllotalpa una midomo miwili kwenye uso wa ardhi ambayo huongoza katika maumbo ya mbiu ambayo huunganisha kwenye upenyo mmoja. Kisha balbu inafuata ambayo inavumisha sauti na mbele yake upenyo wa kutoroka. Upenyo aina hii hutumiwa kwa angalau wiki moja. Dume anajiweka kichwa chini na katika balbu, na mkia wake uko karibu na panda ya upenyo. Spishi nyingine hujenga mbiu moja inayojifungua nje.
Kupandana hufanyika katika upenyo wa dume. Labda dume atapanua upenyo kumpatia jike nafasi ya kumpanda dume, ingawa katika spishi nyingine mjamiiano hufanyika mkia-mkia. Majike hutaga mayai yao katika penyo zao za kawaida au katika vyumba wanvyochimba kwa kusudi hili. Halafu chumba kinafungwa kabisa kwa kisa cha jenasi ya Neoscapteriscus au kutokufungwa kwa kisa cha jenasi Gryllotalpa na Neocurtilla.
Sauti
haririMadume wa chenene hupiga sauti kutoka chini ya ardhi. Kila spishi ina sauti yake ya kipekee. Katika Gryllotalpa gryllotalpa sauti inategemea toni safi karibu na kHz 3.5 iliyo kubwa ya kutosha ili kufanya ardhi itetemeke sm 20 pande zote za upenyo. Katika G. africana marudio ni karibu na kHz 2.34.
Chenene hufanya sauti kama nyenje kwa kukwaruza makali ya nyuma ya bawa la kushoto la mbele, ambalo huunda plectrum, dhidi ya uso wa chini wa bawa la kulia la mbele, ambalo lina safu za meno yasiyo malinganifu; ncha zao zinaelekea nyuma. Plectrum inaweza kusonga mbele kwa nguvu kinzi ndogo, lakini ikisonga nyuma inagusa kila jino, ambayo inasababisha mtetemo katika mabawa yote mawili. Sauti inayosababishwa inafanana na matokeo ya kurekebisha sauti safi kwa wimbi la Hz 66 ili kuunda milio iliyofuatana kwa muda mdogo sawa. Sauti inaweza kulia sana na inaweza kusikika hadi umbali wa m 600 kulingana na spishi. Sauti kubwa zaidi zilizopimwa (kwa G. vineae) zilikuwa na nguvu ya wastani ya desibeli 88 kwa umbali wa m 1 kutoka kwa mdomo wa upenyo. Katika mdomo wake sauti inaweza hata kufikia karibu na desibeli 115. Sauti za G. africana ziko katika mpangilio wa desibeli 94 kwa cm 20 kutoka upenyo.
Koo la mbiu linaonekana kama limerekebishwa ili kufanyia upenyo upeleke sauti vifanisi. Ufanisi huongezeka wakati upenyo ni mnyevu na inasharabu sauti ndogo. Chenene ni wadudu pekee ambao hujenga kifaa cha kuzalisha sauti. Kwa kuzingatia usikivu unaojuliwa wa usikiaji wa chenene kwa desibeli 60, jike la G. africana anayeruka usiku angeweza kugundua sauti ya dume kwa umbali wa m 25-30. Hii inalinganishwa na takriban m 5 kwa nyenje wa jenasi Gryllus ambaye hajengi upenyo.
Ukubwa wa sauti umeunganishwa na ukubwa wa dume na ubora wa makazi, vitu viwili vilivyo viashirio vya uvutivu wa kiume. Madume wenye sauti kubwa wanaweza kuvutia majike 20 kwa jioni moja, wakati dume wenye sauti ndogo atakosa kuvutia hata mmoja. Tabia hii inawezesha utegaji kwa njia ya sauti. Majike wanaweza kutegwa kwa idadi kubwa kwa njia ya kutangaza sauti ya dume kwa ukubwa wa juu.
Chakula
haririChenene hutofautiana katika mlo wao. Wengine, kama chenene wa Ulaya, ni walamani na wengine, kama chenene wa kawaida, hula vitu vingi na kujilisha kwa mabuu, nyungunyungu, mizizi na nyasi. Spishi chache ni mbuai hasa. Huondoka penyo zao usiku ili kutafuta majani na mashina ambayo huvuta chini ya ardhi kabla ya kuyala, na pia hula mizizi na invertebrata chini ya ardhi.
Kama wasumbufu
haririHasara inayosababishwa na chenene ni hasa matokeo ya shughuli zao za kuchimba. Wakipenya kwenye sentimita chache za juu za udongo, wanasukuma ardhi katika matuta madogo, ambayo inaongeza uvukizaji wa unyevu wa uso wa ardhi, kusumbua mbegu zinazoota na kuharibu mizizi dhaifu ya miche. Pia wanaharibu nyasi za nyanja na za machungani kwani wanajilisha kwa mizizi yao na kuifanyia mimea ikauke rahisi na kuharibiwa kwa matumizi.
Katika nchi zao za asili chenene wana maadui wa asili wanaowadhibiti. Hiyo siyo hivyo ikiwa wamewasilishwa kwa bahati mbaya kwenye sehemu nyingine za dunia. Huko Florida, kutoka miaka ya 1940 hadi 1980, walizingatiwa wadudu wasumbufu na walielezewa kama “shida kubwa”. Tangu wakati ule msongamano wa wadudu umepunguka sana. Ripoti ya Chuo Kikuu cha Florida kuhusu wadudu hao inadokeza kwamba chenene wa Neoscapteriscus wa Amerika ya Kusini waliingia Marekani labda huko Brunswick, Georgia, katika farumi ya meli kutoka kusini kwa Amerika ya Kusini mnamo 1899, lakini wakati huo ilidhaniwa kimakosa kwamba walitoka kwenye Visiwa vya Karibi. Utatuzi mmoja unaowezekana ulikuwa udhibiti wa kibiolojia wa wasumbufu kwa kutumia nyigu kidusia Larra bicolor. Utatuzi wingine uliotumika kwa mafanikio ni matumizi ya nematodi kidusia Steinernema scapterisci. Wakinyunyiziwa kwenye vishoroba vipitavyo uwanja wa nyasi wanaenea katika machungani yote (na labda mbali zaidi) ndani ya miezi michache ijayo na hawadhibiti chenene sasa hivi tu lakini pia wanabaki tayari kuambukiza katika udongo kwa muda wa miaka kadhaa.
Spishi za Afrika
hariri- Gryllotalpa africanus, Chenene wa Kawaida
- Gryllotalpa brevilyra
- Gryllotalpa bulla
- Gryllotalpa cossyrensis
- Gryllotalpa debilis
- Gryllotalpa devia
- Gryllotalpa elegans
- Gryllotalpa gryllotalpa, Chenene wa Ulaya
- Gryllotalpa madecassa, Chenene wa Madagaska
- Gryllotalpa maroccana, Chenene wa Maroko
- Gryllotalpa microptera, Chenene Mabawa-mafupi
- Gryllotalpa parva
- Gryllotalpa pluridens
- Gryllotalpa robusta
- Gryllotalpa rufescens
- Gryllotalpa spissidens
- Gryllotalpa weisei
Picha
hariri-
Chenene wa Ulaya
-
Oriental mole cricket (Gryllotalpa orientalis)
-
Northern mole cricket (Neocurtilla hexadactyla)
-
Southern mole cricket (Scapteriscus borellii)