Hafez
Makala hii inamhusu mshairi Mwajemi, Kwa maana mengine ya neno Hafez / Hafiz angalia Hafiz (maana)
Khwajeh Shams al-Din Muhammad Hafez-e Shirazi ( خواجه شمسالدین محمد حافظ شیرازی) (* mnamo 1319 mjini Shiraz; † mnamo 1389 akiwa na umri wa miaka 69) anayejulikana kwa kawaida kwa kifupi kama Hafez (pia Hafiz) anajulikana kama mshairi muhimu wa Uajemi. "Hafez" ilikuwa jina lake la heshima kwa sababu alijua Qurani yote tangu utotoni maana yake ni sawa na Kiswahili hafiz yaani mtu anayeshika Qurani yote moyoni. Mashairi yake yanapendwa sana hadi leo nchini Uajemi na kitabu chake kinachoitwa Divan-e Hafez kinapatikana katika familia nyingi za nchi hii. Wengi wameyashika na wakati wa sikukuu mbalimbali Waajemi wanayasoma. Kaburi lake hutembelewa sana na Waajemi wengi wanasafiri kutembelea mji wa Shiraz hasa kwa kuona kaburi lake.
Mashairi yake yanahusu mara nyingi habari za mapenzi, divai na ulevi yakipinga unafiki wa hao wanaojiita watunzi wa maadili katika jamii.
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Habari za maisha yake hazina uhakika; mengi ni masimulizi tu zenye tabia za hekaya.
Baba yake aliitwa Baha-ud-Din alikuwa mwuzaji wa makaa akafa Hafez alipokuwa mdogo. Mvulana alivutwa sana na kumbukumbu jinsi baba alisoma Qurani akajitahidi akaweza kushika Qurani yote alipokuwa na umri wa miaka 8. Lakini alisikia pia mashairi ya Maulana Rumi na Sa'di. Inaaminiwa ya kwamba alipata mafundisho katika madrasa.
Hafez alitangulia kazi ya kuoka mkate hadi umri wa miaka 21 alipokuwa mwanafunzi wa mshairi Fariduddin Attar. Wakati wa kupeleka mikate yake kwa wateja alipata kumjua mama mmoja membo sana kwa jina Shakh-e Nabat akatunga shairi zake za kwanza kwa ajili yake na uzuri wake. Alipotambua ya kwamba hawezi kuwa pamoja naye alitambua upotovu wa urembo akaanza kuimbia uzuri wa ndani au kiroho.
Alijulikana akaajiriwa na mtawala wa Shiraz kama mshairi wa ikulu yake. Mnamo 1333 mji ulivamiwa na maadui na Hafez aliachishwa kwenye ikulu. Aliendelea kutunga mashairi na kufundisha.
Hadithi moja inamkumbuka akiwa na umri wa miaka 60 akachora duara chini na kuketi ndani yake kwa siku 40 akitafakari maisha, dunia na Mungu. Inasemekana ya kwamba mwishoni aliona nuru ya ndani baada ya kumaliza kikombe cha divai.
Aliaga dunia akiwa na miaka 69 na msahiri mheshimiwa na wengi.
Kazi
[hariri | hariri chanzo]Hakuna uhakika juu ya idadi ya masahiri yake. Matoleo mbalimbali huwa kati ya masahiri 573 hadi 994. Wajemi wanapenda kutumia mashairi yake kwa aina ya utabiri wakifungua kitabu mahali popote na kuchukua ayat zilizopo hapa kama jibu kwa swali fulani.
Utamaduni wa Hafez ilikuwa Uislamu lakini anaheshimiwa na kusomew pia na Wahindu na Wakristo. Waislamu waliona matatizo katika sifa zake za divai hivyo walizoea kusoma ayat zake kama lugha ya kishairi yenye picha lakin watu wasio Waislamu walifurahia pia kuona ushairi unaounganisha maono ya kiroho na sifa za divai.