(Translated by https://www.hiragana.jp/)
Mmea - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Mmea

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Planta)
Aina mbalimbali za mimea.

Mimea (kwa Kiingereza: "plants", kutoka Kilatini "Plantae") ni moja kati ya makundi ya viumbe hai duniani likijumuisha miti, maua, mitishamba na kadhalika. Kuna zaidi ya aina 300,000 ya mimea.

Sayansi inayochunguza mimea huitwa botania ambayo ni kitengo cha biolojia. Kwenye uainishaji wa kisayansi mimea hujumlishwa katika himaya ya plantae kwenye milki ya Eukaryota (viumbehai vyenye kiini cha seli na utando wa seli).

Kwa hiyo mimea huwa na utando wa seli wenye selulosi. Mmea unapata sehemu kubwa ya nishati kutoka nuru ya jua kwa njia ya usanisinuru, yaani hujilisha kwa msaada wa nuru. Ndani ya majani ya mimea kuna klorofili, dutu ya rangi ya kijani, inayofanya kazi ya kupokea nuru na kupitisha nishati yake kwa sehemu nyingine ya mmea ambamo inatumiwa kujenga molekuli zinazotunza nishati kwa njia ya kikemia na kutumiwa katika metaboli ya mwili.

Mimea kadhaa imepoteza uwezo wa kutengeneza klorofili ya kutosha, hivyo inajipatia nishati kama vimelea kutoka kwa mimea au viumbehai wengine.

Mimea mingi inazaa kwa njia ya jinsia, yaani kwa kuunganisha seli za kiume na kike; mara nyingi viungo vya kiume na vya kike vinapatikana ndani ya mmea mmoja. Kuna pia mimea inayozaa kwa njia isiyo ya kijinsia, kwa mfano kwa kuotesha mzizi wa hewani ambao unaingia ardhini na kuendelea kama mmea wa pekee.

Mimea ni msingi muhimu kwa viumbehai wengine duniani kwa sababu sehemu kubwa ya oksijeni katika angahewa ya dunia inatengenezwa na mimea.[1].

Mimea inatoa chakula kwa binadamu kama vile nafaka, matunda na mboga za majani, pia lishe kwa wanyama wa kufugwa.

  1. Field, C.B.; Behrenfeld, M.J.; Randerson, J.T.; Falkowski, P. (1998). "Primary production of the biosphere: Integrating terrestrial and oceanic components". Science. 281 (5374): 237–240. Bibcode:1998Sci...281..237F. doi:10.1126/science.281.5374.237. PMID 9657713.
Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mmea kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.