Mofimu
Mofimu ni kipashio kidogo kuliko vyote katika lugha chenye maana ya kisarufi /kileksika. Mofimu katika sarufi ni jina la sehemu ndogo kabisa yenye kuwakilisha maana katika neno. Kipashio hiki hakiwezi kuvunjwavunjwa zaidi bila kupoteza maana. Mfano:
- "Analima" - A-na-lim-a
Neno analima lina mofimu nne ambazo hufungamana na kujenga neno analima. Kila moja ya mofimu hizi isimamapo pekee haina maana yoyote isipokuwa ina maana kisarufi ambayo humwezesha mwanaisimu kuchambua maana hiyo.[1]
Mifano ya jumla
- neno "nimefika" (kitenzi) lina pia mofimu nne ndani yake:
- "ni" - ni mofimu ya nafsi ya kwanza ya umoja
- "me" - ni mofimu ya wakati / halinjeo
- "fik" - ni kiini cha tendo / kitenzi
- "a" - inaonyesha nia / kiambishi tamati
Aina za mofimu
Kuna aina kuu mbili za mofimu nazo ni:
- Mofimu huru
- Mofimu Tegemezi/Funge /Ambata
Mofimu huru
Mofimu huru ni silabi moja au zaidi yenye maana kamili ya neno na inaweza kujisimamia bila msaada wa viambishi au silabi nyingine. Aghalabu mofimu huru huwa nomino, vivumishi au vielezi visivyochukua viambishi vya ngeli. Kwa mfano:
- Daktari
- Ndoa
- Nyumba
Mofimu tegemezi/funge/ambata
Mofimu tegemezi huhitaji viambishi au mofimu nyingine tegemezi ili kuleta maana iliyokusudiwa. Mofimu hizi hujumuisha hasa mzizi wa neno (au shina la kitenzi), vivumishi, nomino au vielezi ambavyo vinahitaji viambishi viwakilishi vya ngeli ili kutoa maana iliyokusudiwa.
Shina la kitenzi au mzizi wa neno au kiini cha kitendo ni sehemu ndogo zaidi inayosimamia kitenzi chenyewe bila mnyambuliko, nyakati au viambishi vinginevyo.
Viambishi ni mofimu tegemezi ya silabi moja inayowakilisha dhana fulani kama vile hali, ngeli, nafsi, wakati na kadhalika.
- Kwa mfano
- m-tangaz-a-ji
- wa-me-tu-sumbu-a
- wa-ku-lim-a
- m - mofimu ya ngeli ya M-WA kwa umoja
- tangaz - mzizi wa neno, kiini cha kitendo cha kutangaza
- a - kiishio cha kitenzi
- ji - inaonyesha kazi au mazoea
- a - kiishio cha kitenzi
- tangaz - mzizi wa neno, kiini cha kitendo cha kutangaza
- m - mofimu ya ngeli ya M-WA kwa umoja
- wa - kiambishi kiwakilishi cha nafsi ya tatu
- me - kiambishi cha wakati timilifu
- tu - kiambishi kiwakilishi cha nafsi ya kwanza wingi - kitendewa/mtendwa
- sumbu - shina la kitendo cha kusumbua
- a - kiishio
Marejeo
- ↑ J.A. Masebo na Nyambari Nyangwine 2012, "Jitayarishe kwa Kiswahili", "Chapa ya Pili" - ISBN 978 9987 09 017 4